

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Tabora Kepteni Mstaafu Ukiwaona Ditopile Mzuzuri aliyefariki jana Aprili 20,2008 majira ya saa 3:00 katika Hotel ya Hilux iliyopo Mkoani Morogoro anatarajiwa kuzikwa kesho huko Kinyerezi, pembezoni mwa jiji la Dar, maeneo ya Segerea.
Mamia ya waombolezaji wamefurika nyumbani kwa mareehemu mtaa wa Mindu, Upanga, Dar, kujiunga na familia ya marehemu katika kuomboleza kifo hicho ambacho kimeacha watu wengi midomo wazi
Marehemu Ditopile alifikia katika hoteli ya Hilux ,Morogoro akitokea Tabora akiwa safarini kuelekea Dar es Salaam kwa mapumziko akiwa ameambatana na mkewe mdogo,Tabia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa hoteli hiyo Joseph Kitambi, Ditopile alifika hotelini hapo Aprili 18, majira ya saa 5:30 usiku,ambapo alipatiwa chumba No.106.
Kitambi alisema Aprili 19,majira ya saa 5:00 usiku watumishi wa hoteli hiyo wakati wakifunga shughuli zao za huduma, Ditopile alikuwa bado hajarudi hotelini kutoka kwenye shughuli zake ambazo amekuwa akizifanya kwa muda wote tangu kufika hotelini hapo.
Akifafanua zaidi Mkurugenzi huyo alisema, Aprili 20 majira ya saa 2:30 asubuhi mkewe Tabia alitoa taarifa ya kuzidiwa kwa mumewe na kuomba msaada ambapo wahudumu walifika katika chumba chake na kumwangalia na kukuta akiwa amelala kwenye kochi,na alionekana kuwa ni mtu asiyejitambua,na kutoa taarifa kwenye hospitali kuu ya Mkoa kwa msaada zaidi.
Mkurugenzi huyo aliiambia habari leo kuwa marehemu alifariki kabla ya kupata kifungua kinywa cha asubuhi ambacho hutolewa na hoteli hiyo kuanzia saa 12:30 asubuhi hadi majira ya saa 4:30.
Alisema kuwa wauguzi wa hospital walifika katika hoteli hiyo,na kumchukua kwenye gari,akionekana kama mtu ambaye ameshafariki,na kumpeleka hospitalini kwa ajili ya kufanya uchunguzi zaidi.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo alidai kwa kipindi chote ambacho Ditopile amekuwa katika hoteli hiyo,alionekana kuwa ni mtu aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi,kutokana na mwili wake kudhoofu na nyuso kutokuwa na uchangamfu.
Aidha alidai kuwa wakati wafanyakazi hao wanautoa mwili wake nje kwa kushirikiana na madaktari waliofika kutoka hospitalini,walikuta mswala wa kuswalia,ambapo mkewe alidai kuwa mumewe aliamka alfajiri na kuswali swala ya asubuhi,kabla ya mauti kumkuta.
Baada ya mwili huo kufikishwa hospitalini Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa Dkt.Meshack Masi alisema alipokea taarifa kutoka kwenye uongozi wa hoteli hiyo,iliyoeleza kuwa Ditopile amezidiwa hivyo wanahitaji msaada haraka.
'Kweli tulipokea taarifa hizo…walikuwa wakiomba msaada haraka…na sisi tulituma gari pamoja na wauguzi mara moja kwenda pale Hilux hoteli na kumleta hapa hospitalini'alisema Daktari Masi.
Hata hivyo Dkt.Masi alisema baada ya wauguzi kufika hotelini hapo,na kuuona mwili wake waligundua kuwa ameshafariki na kuubeba mwili wake na kuupeleka hospitalini hapo na kuulaza wodini grade 1, kwa ajili ya kuudhibitisha,kabla ya kuupeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Thobias Andengenye alisema kuwa marehemu alipotoka mkoani Tabora alifika Mkoani Morogoro na kwenda Wilaya ya Mvomero kwa ajili ya kukagua mashamba yake yaliyopo kwenye eneo la Mgongola akiwa na mkewe mdogo Tabia kabla ya kufika Morogoro Mjini ambapo alipata malazi.
Aliongeza kuwa baada ya kukagua mashamba yake marehemu aliondoka Wilayani Mvomero na kuja Morogoro Mjini ambapo alifika majira ya saa 3 usiku na kufikia kwenye hotel ya Hilux iliyopo Mjini hapo kwa ajili ya kupata malazi ambapo alipewa chumba No.106.
Alisema marehemu aliitumia siku ya Aprili 19,kutembelea ndugu na jamaa zake kabla ya kurudi nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam,na kudai kuwa alirudi hotelini hapo majira ya saa 12 jioni,ambapo alitarajia kuondoka Aprili 20 kurudi nyumbani kwake.
Katika ziara ya marehemu ya kutembelea na kusalimiana na ndugu zake,pia alipata wasaa wa kumtembelea Chifu Kingalu Mwana Banzi wa 14 wa kabila la waluguru.
Kwa upande mwingine mdogo wake na Marehemu, Selemani Mzuzuri,alipohojiwa alisema hana lolote la kuzungumza na kueleza kuwa bado ana majonzi mazito ya kifo cha kaka yake,hivyo hataweza kuzungumzia jambo lolote.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Meja Jeneral mstaafu Said Kalembo ambaye alifika hospitali ya mkoa wa Morogoro akizungumza na waandishi wa habari alisema kwamba mwili wa marehemu unatarajiwa kuchukuliwa na gari la jeshi na kusafirishwa kuupeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kwenye hospitali ya Jeshi ya Lugalo iliyopo Dar es salaam.
Marehemu Ditopile, ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, amewahi pia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,Lindi na Tabora kabla ya kukabiliwa na kesi ya Mauaji bila kukusudia.

0 Comments