Rais Jakaya Mrisho Kikwete amepewa wadhifa wa uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) na katika jitihada zake za kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili amehutubia kikao cha wakuu wa nchi za wanachama wa umoja huo kwa lugha hiyo. Katika makala haya, Hamis Mzee, anaangalia lugha hiyo na umuhimu wake kwa maendeleo na ustawi wa jamii kwa jumla.
Licha ya kutumiwa na watu zaidi ya milioni 100 wa nchi za Afrika mashariki za Tanzania, Kenya na Uganda na kati kama Jamhuri ya Kongo pamoja na baadhi ya wakazi wa nchi za Kusini kama Msumbiji, Kiswahili ni lugha inayopewa kisogo hasa na viongozi, wasomi na watumiaji wa lugha za kigeni zilizokuzwa kihistoria kutokana na kutawaliwa na wakoloni.
Katika nchi nyingi za Afrika licha ya wananchi wake kuwa na lugha zao za mawasiliano za kiasili, lugha zinazotukuzwa na kupewa umuhimu ni zile za nje za Kiingereza, Kifaransa na Kireno.
Kwa Waafrika kusini mwa jangwa la Sahara, matumizi ya lugha za kigeni yamekuwa yakikuzwa kwa sababu mbalimbali mojawapo ni kukosekana lugha ya kuunganisha watu wengi wa makabila tofauti.
Ingawa katika baadhi ya nchi zipo lugha zinazozungumzwa na wengi na hata wakati mwingine kutumiwa na zaidi ya nchi moja, kumekuwa na vikwazo katika kuziendeleza lugha hizo.
Katika nchi zingine, lugha zinazotumiwa na watu wa kawaida zimeishia kuwa za mitaani tu kwa kuwa hazitumiwi hata na vyombo vya habari!
Nchi za Kaskazini za Afrika ambazo karibu zote ni za kiarabu zilibaini mapema umuhimu wa kukuza na kutukuza kiarabu na zimekuwa zikitumia lugha hiyo hata katika mikutano ya kimataifa.
Imekuwa ni bahati nzuri kuwa Kiswahili lugha inayotumiwa Tanzania na kwa kiasi, nchi zingine za Afrika Mashariki imepewa uzito na umaarufu kwa kukubaliwa kuwa moja ya lugha rasmi zinazotumika katika Umoja wa Afrika.
Pamoja na ukweli huo, kukubalika pekee kama lugha rasmi ya kutumia katika Umoja wa Afrika hakutoshi ikiwa hakuna wanaokitumia.
Ingawa Tanzania ndiyo Kiswahili kinatumika sana kwa mawasiliano ya wananchi na hata rasmi kiserikali, cha kushangaza rais aliyetumia Kiswahili kwa mara ya kwanza hakuwa wa Tanzania!
Alikuwa Rais Joaquim Chissano wa Msumbiji aliyezungumza wakati akimaliza muda wake kama mwenyekiti wa umoja huo.
Kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza wakati kiongozi huyo alipozungumza kwenye mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa AU mwaka 2004, ripoti zinadai hakukuwa na wakalimani na hivyo kumfanya kiongozi huyo wa Msumbiji kutafsiri mwenyewe alichokuwa akisema kwa Kiswahili.
Mpaka wakati huo katika Umoja wa Afrika ama AU lugha rasmi zilikuwa ni Kiarabu, Kireno, Kifaransa na Kiingreza.
Rais Chissano ambaye sasa ni mstaafu alisema ametumia Kiswahili kwa lengo ya kukuza utambulisho wa waafrika na lugha zao.
Wakati Rais Chissano alipozungumza Kiswahili kwa mara ya kwanza viongozi wengi na hata mabalozi walipatwa na mshangao. Kikao hicho kilikikubali Kiswahili mojawapo ya lugha rasmi za umoja huo.
Kuanzia wakati huo Kiswahili kimepata msukumo na hatua ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuhutubia wakuu wa nchi wanachama wa AU kwa Kiswahili wakati akihutubia kama Mwenyekiti wao bila shaka inakuza dhamira ya kukikuza na kukiboresha Kiswahili kama mojawapo ya lugha rasmi za Umoja huo.
Rais Kikwete ambaye amechukua uenyekiti wa AU kutoka mwenyekiti aliyemaliza muda wake Rais John Kufuor wa Ghana, aliwafurahisha wakuu wenzake waliohudria mkutano wa wiki iliyopita kwa kuwaambia kuwa atawahutubia kwa Kiswahili.
Alipoanza kuhutubia alisababisha kicheko zaidi pale alipokatisha na kuulizia kama wanapata tafsiri katika lugha walizozoea za Kifaransa, Kiingereza na Kireno?
Hatua hiyo ya Rais Kikwete kama Mwenyekiti wa AU bila shaka ni ujasiri wa kipekee kwani imekuwa mazoea kwa wakubwa wanapokutana kutumia lugha za kigeni na kuonyeshana umahiri wao wa lugha hizo.
Msimamo wa Kikwete wa kupigia debe Kiswahili si mgeni kwani mara nyingi hata kwenye mikutano hapa nchini amekuwa akihimiza watu kuchangamkia Kiswahili kwani ni lugha inayokua na ina ajira tosha kwani walimu na wakalimani wanahitajika katika nchi mbalimbali.
Kwa uamuzi wake wa kutumia Kiswahili katika kikao cha majuzi cha AU mjini Addis Ababa, Ethiopia bila shaka atakuwa amewafurahisha wakalimani wa Kiswahili ambao bila kuwa na mzungumzaji wa lugha hiyo wangekuwa hawana kazi ya kufanya.
Wakati tukishangilia maamuzi haya ya kukikuza Kiswahili hata kwenye chombo chenye hadhi katika bara la Afrika cha Umoja wa Afrika, ni muhimu tukaangalia na kutafakari nafasi ya Kiswahili hasa katika maeneo muhimu hapa nchini.
Ni vizuri kutafakari zaidi kuangalia uwezekano wa Kiswahili kutumika kama lugha ya kufundishia katika elimu ya juu bila ya kuathiri lugha za kigeni.
Kama wenzetu katika nchi zingine kama za kiarabu na zingine wameweza kutumia lugha zao kwa elimu ya juu na huku wakiendeleza pia ufundishaji wa lugha za kigeni, kwanini hapa iwe shida?
Kutokana na kukua kwa Kiswahili hata kampuni ya kompyuta Microsoft imechukua hatua ya kuwa na programu ya kompyuta ya Kiswahili.
Habari zinaeleza kuwa kampuni hiyo kubwa ya kompyuta pia inataka kuwa na kutoa programme ya Windows kwa lugha zingine za Afrika kwa lengo la kuzuia lugha hizo zisimezwe na Kiingereza!
Ni wazi hawa wanafanya hivi kwa biashara na kwa sababu wanaona wapo wateja.
Hata hivyo ni ukweli ulio wazi lakini unaopuuzwa kuwa lugha zetu hasa Kiswahili kimepanuka hivyo kitumike ipasavyo kuleta umoja, mshikamano na maendeleo kwani upo usemi kuwa mtu hawezi kupata maendeleo kwa lugha ya kuazima! style="font-weight:bold;">
0 Comments