SHEREHE ZA MUUNGANO KUTIMIZA MIAKA 44 ZIMEFANA SANA

Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama leo amewaongoza Watanzania katika sherehe za kufana za kuadhimisha miaka 44 ya Muungano wa Tanzania.

Ilikuwa tarehe 26 Aprili 1964 wakati Tanzania Bara wakati huo Tanganyika ilipoungana na Zanzibar baada ya mapinduzi yake ya tarehe 12 Januari 1964 na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati wa sherehe zilizofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Rais Kikwete aliingia uwanjani akiwa kwenye gari la wazi la Amiri Jeshi Mkuu akifuatana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange na kuzuka uwanja kuwasilimia watu kwa kuwapungua mkono.

Baadaye alikwenda kwenye jukwaa kupokea saluti na kupigiwa mizinga 21 huku wimbo wa taifa ukipigwa na hatimaye kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na vikosi sita vya majeshi ya ulinzi na usalama.

Baadaye vikosi vya gwaride kuu lililokuwa nje viliingia uwanjani na kupita mbele ya Rais na kufuatiwa na gadi maalum ya kivita kikiwemo kikosi cha makomando, ndege za kijeshi za helikopita, usafirishaji na kivita na sherehe kuhitimishwa kwa halaiki na ngoma mbali mbali.

Wakati huo huo katika kuadhimisha miaka 44 ya Muungano wa Tanzania Rais Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa wapatao 3,368.

Miongoni mwa wafungwa waliofaidika na msamaha huo ni wale wanaotumikia kifungo kisichozidi miaka mitano ambao hadi leo watakuwa wametumikia robo ya vifuo vyao.

Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Lawrence Masha wengine ni wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama ukimwi, kifua kikuu na saratani walioko katika hali mbaya.

Wengine ni wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini au zaidi, wafungwa wa kike walioingia na mamba gerezani au watoto wachanga wanaonyonya na wafungwa walemavu wa mwili na akili.

Hata hivyo msamaha huo hautawahusu wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, wanaotumika kifungo cha maisha, wenye makosa ya madawa ya kulevya na kupokea au kutoa rushwa.

Wengine ni pamoja na wale wenye makosa ya kupatikana na silaha, makosa ya kujamiiana, wizi wa magari kwa kutumia silaha na kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na hivyo kushindwa kuendelea na masomo.

Post a Comment

0 Comments