BUSH NDANI YA BONGO FLAVA

Karibu Rais George Bush
2008-02-16 08:44:06
Na Mhariri

Rais Geroge Walker Bush wa Marekani, anawasili nchini leo kwa ziara ya siku nne.

Zaidi ya Tanzania, Rais Bush atazitembelea pia nchi za Rwanda, Benin, Ghana na Liberia, ambapo kati ya hizo, hakuna nchi atakayokaa kwa muda mrefu kama ilivyo Tanzania.

Hivyo, hatua ya kukaa nchini kwa muda huo ambao hata mtangulizi wake, Rais mstaafu wa Marekani, Bw. Bill Clinton, hakuutumia alipotembelea Tanzania, inaashiria mambo mengi na makubwa.

Wapo wanaoweza kutaja ukarimu wa Watanzania unavyojulikana, amani na utulivu uliopo, mipango na mikakati endelevu ya ukuaji wa uchumi, kwamba ni miongoni mwa sababu za Rais Bush kuja na kukaa kwa muda mrefu. Wote hao wapo sahihi.

Ni vizuri tukatamka wazi kwamba ujio wa Rais Bush unapaswa kuungwa mkono na watu wa kada na itikadi zote, kutokana na ukweli kwamba, malengo yake yana manufaa kwa Taifa na watu wake.

Tuna kila sababu ya kuushawishi umma wa Watanzania kujitokeza kwa wingi kumpokea kiongozi huyo kutoka Taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi na kijeshi, kutokana na ukweli unaohalalishwa na matukio ya ushirikiano kati ya nchi mbili hizi.

Takwimu zinaonyesha wazi kwamba Marekani ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa utoaji wa misaada inayoelekezwa katika sekta za afya, miundombinu na maendeleo kwa ujumla hapa nchini.

Ni vizuri Watanzania wakazingatia kwamba chini ya uongozi wa Rais Bush, Tanzania ilifanikiwa kupata msaada wa fedha kupitia vyanzo mbalimbali, ikiwamo Mfuko wa Changamoto ya Milenia (MCC), Mpango wa Dharura wa Kupunguza Makali ya Ukimwi (PEPFAR), Mpango wa Kupambana na Malaria (PMI).

Zaidi ya hayo, kuna mashirika ya Kimarekani yanayotoa huduma za kijamii nchini, huku yakitegemea fedha kutoka vyanzo mbalimbali, lakini kwa sehemu kubwa ikiwa ni Serikali ya Marekani.

Aidha, hivi sasa kuna Watanzania wengi wanaosoma ama kufanya kazi nchini Marekani.

Hatujawahi kupata taarifa zozote zinazohusiana na unyanyaswaji, uonevu ama ubaguzi wanaofanyiwa Watanzania hao huko Marekani.

Kwa hiyo tunapoitazama Marekani na ushirikiano wake na Tanzania tunapata faraja kwamba Rais Bush anakuja kuimarisha ushirikiano huo.

Bila shaka ujio wa Rais Bush utapanua milango ya wawekezaji wa Marekeni kuja kuwekeza Tanzania na Watanzania kwenda kusoma na kufanya kazi Marekani.

Aidha, ujio wa Rais Bush ni nafasi pekee ya kuitangaza nchi yetu duniani kote.

Anaambatana na waandishi wa habari wapatao 100 na anatembelea sehemu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na baadhi ya vivutio vya watalii hapa nchini.
Tunaamini kabisa kwamba huu ni wakati muafaka wa kuonyesha walimwengu ukarimu wetu na vivutio vya watalii katika nchi yetu kwa kupitia waandishi na maofisa wengine atakaofuatana nao.

Pamoja na manufaa tuliyoyataja hapo juu, Tanzania ni nchi inayotumika kama kielelezo cha ustaarabu barani Afrika, hivyo mapokezi ya Rais Bush yanapaswa kutumika kama fursa ya kuuonyesha ulimwengu kuhusu ukweli huo.

Kwa sababu hiyo, tunaungana na Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Sheikh Mkuu wa Tanzania , Mufti Shaaban bin Simba, kuwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais Bush leo.

Vifijo,shangwe na vigelegele vitawale kote atakapopita.

Kwa mara nyingine tena tunasema KARIBU SANA TANZANIA Rais George Walker Bush

Post a Comment

0 Comments